Muhogo Wa Jang'ombe

 

Muhogo wa Jang'ombe, sijauramba mwiko

Usitukane wakunga, na uzazi ungaliko
Kaditamati naapa, muhogo sitonunua
Haikuwa Maimuna, aliyekwenda ung'oa
Kapata tete kuanga, na ugonjwa wa shurua

Kula dori kula dori, mshindo wa sufuria
Guliguli guliguli, kofia ina viua
Ndiye mimi ndiye mimi, anipataye ukoa

Mungu akitaka kupa, hakuletei barua
Hukupa usingizini, pasi mwenyewe kujua
Kwenda mbio sikupata, bure unajisumbua

Mkato wake matege, wakati anapokuja
Naliiweka dhamiri, ya kumfulia koja
Wallahi nimeghairi, kiumbe hana mmoja

Kamfunge kamfunge, beberu wa Athumani
Umfunge umfunge, pahala panapo jani
Endaye tezi na omo, atarejea ngamani

Sina ngoa sina ngoa, kuhadaiwa sitaki
Ni mwerevu ni mwerevu, wala sihadaiki
Pambanua pambanua, viwili havipendeki

Ya nini kutakadamu, kwa jambo lisilokuwa
Utahadhari na mwiko, wakati wa kupakua
Ukitamani makoko, chungu utakitoboa

Nauliza masuala, hamnambii jamani
Watu wake wakishiba, huzidi umaluuni
Pahala pasipo ngoma, hupandwaje na shetani
Nyimbo ya Bi Kidude
Imeletwa na Hassan O. Ali

Enregistrer un commentaire

0 Commentaires

Uso cookies para darte un mejor servicio.
Mi sitio web utiliza cookies para mejorar tu experiencia. Acepto Leer más